Maelezo ya Jumla

Jukwaa la uchukuaji wa hatua 

Maadhimisho ya nne ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na Anga za Bluu yatafanyika tarehe 7 Septemba mwaka wa 2023; mipango na maandalizi ya maadhimisho yake tayari inaendelea.

Inaangazia umuhimu wa kuwa na ushirikiano thabiti, kuimarisha uwekezaji na uwajibikaji wa pamoja ili kukomesha uchafuzi wa hewa. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitenga tarehe 7 Septemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za buluu katika mwaka  wa 2019, na maadhimisho ya kwanza yalifanyika mwaka wa 2020. Hii inafuatia ongezeko la uelewa wa jamii ya kimataifa kuhusu hatari za uchafuzi wa hewa na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kuboresha hali ya hewa ili kutunza afya ya binadamu na hali ya mazingira.

Uchafuzi wa hewa ni tishio la mazingira sio tu kwa afya ya binadamu, bali pia kwa hali ya sayari. Una madhara mabaya kwa hali ya hewa, bayoanuai na kwa mifumo ya ekolojia. Kuboresha hali ya hewa yetu kutaleta manufaa kwa afya, maendeleo na kwa mazingira.

Wakati huu wa Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu, tunatoa wito kwa kila mtu, serikali, mashirika, mashirika ya uraia na watu binafsi kushirikiana kupunguza uchafuzi wa hewa na kuleta mabadiliko chanya ya kuwezesha kuwa na hewa safi kwa wote.

Uchafuzi wa hewa huwaathiri kwa kiwango kikubwa watoto na wazee, na huwa na athari mbaya kwa mifumo ya ekolojia. Kuboresha hali ya hewa ni muhimu ili kukabiliana na athari za vichafuzi vingi vinavyochangia moja kwa moja kwa janga la hali ya hewa na kuimarisha ubora wa hewa kunaweza kupunguza mabadiliko ya tabianchi. Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, pia inatambua kwamba kupunguza uchafuzi wa hewa ni muhimu ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu inakusudia kujenga jamii ya kimataifa ya kuchukua hatua inayohimiza nchi kushirikiana ili kukabiliana na uchafuzi wa hewa ili kuhakikishia kuwa tunatunza mifumo yetu ya ekolojia. Kufanikisha haya, inawapa watu jukwaa linalowezesha ushirikiano katika ngazi ya mtu binafsi, kitaifa, kikanda na kimataifa kufanya kazi #PamojaKuwaNaHewaSafi.