Sababu Za Uchafuzi Wa Hewa

Uchafuzi wa hewa unaweza kutengenezwa katika eneo letu, lakini unaweza kusafiri mbali mno, wakati mwingine katika mabara  kwenye ruwaza za hali ya hewa ya kimataifa.

Hakuna mtu aliye salama kutokana na uchafuzi huu wa mazingira, ambao unatoka kwa vyanzo vitano vikuu kutoka kwa binadamu . Vyanzo hivi huzalisha vitu anuwai ikiwa ni pamoja na kaboni monoksidi, kaboni dioksidi, nitrojeni dioksidi, nitrojeni oksidi, ozoni ya kiwango cha chini, chembe chembe, sulfuri dioksidi, haidrokaboni na risasi - zote ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.

NYUMBANI

Chanzo kikuu cha uchafuzi wa hewa wa nyumbani ni kuchoma fueli ya visukuku ndani ya nyumba, kuni na fueli ingine inayotokana na mimea kupika, kupasha nyumba joto na kutoa mwangaza. Karibu vifo vya mapema milioni 3.8 husababishwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba kila mwaka, idadi kubwa kati ya vifo hivyo ni katika nchi zinazoendelea.
 
Kati ya nchi 193, nchi 97 zimeongeza asilimia ya familia ambazo zinapata fueli isiyochafua mazingira inapochomwa kwa zaidi ya asilimia 85. Hata hivyo, watu bilioni 3 wanaendelea kutumia fueli mango na moto wazi kupika, kupasha joto na kutoa mwangaza. Matumizi ya majiko  ya kisasa zaidi na fueli zisizochafua mazingira kunaweza kupunguza hatari za ugonjwa na kuokoa maisha. 

VIWANDA

Katika nchi nyingi, uzalishaji wa nishati  ni chanzo kinachoongoza cha uchafuzi wa hewa. Mitambo ya kuchoma makaa ya mawe inachangia pakubwa, wakati jenereta za dizeli ni tishio kwa maeneo yasiyofikiwa na umeme. Michakato ya viwanda na matumizi ya viyeyushi, katika viwanda vya kemikali na madini, pia huchafua hewa.
 
Sera na programu zinazolenga kuiarisha ufanisi wa nishati na uzalishaji kutoka kwa vyanzo vinavyoweza kutumika tena ina athari ya moja kwa moja kwa ubora wa hewa ya nchi. Kwa sasa, nchi 82 kati ya 193 zina vichocheo ambavyo vinakuza uwekezaji katika uzalishaji wa nishati inayoweza kutumika tena, uzalishaji usiochafua mazingira, matumizi ya nishati kikamilifu na au udhibiti wa uchafuzi wa mazingira. 

UCHUKUZI

Sekta ya uchukuzi ulimwenguni inawajibikia karibu robo moja  ya uchafuzi unaohusiana na kaboni dioksidi, kiwango ambacho kinazidi kuongezeka. Uchafuzi huu unaotokana na uchukuzi umehusishwa na takribani vifo 400,000 vya mapema. Karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na uchafuzi wa hewa kutoka kwa uchukuzi vinasababishwa na uchafuzi wa dizeli, wakati wale wanaoishi karibu na sehemu kubwa ya trafiki wana uwezekano wa hadi asilimia 12 zaidi  kugunduliwa kuwa na matatizo ya kiakili.
 
Kupunguza uchafuzi kutoka kwa magari ni hatua muhimu ya kuboresha ubora wa hewa, haswa katika maeneo ya mijini. Sera na viwango vinavyohitaji matumizi ya fueli zisizochafua mazingira na viwango vya juu vya uchafuzi wa gari vinaweza kupunguza uchafuzi wa gari kwa asilimia 90 au zaidi.

KILIMO

Kuna vyanzo viwili vikuu vya uchafuzi wa hewa kutoka kwa kilimo: mifugo, ambayo hutoa methani na amonia, na kuchoma taka za kilimo. Uchafuzi wa methani unachangia ozoni ya kiwango cha chini, ambayo husababisha pumu na magonjwa mengine ya mfumo wa kupumulia. Methani pia ni gesi yenye uwezo mkubwa wa kuongeza kiwango cha joto duniani kuliko kaboni dioksidi - athari yake ni kubwa mara 34 zaidi kwa kipindi cha miaka 100. Karibu asilimia 24 ya gesi zote za ukaa zinazotolewa ulimwenguni zinatokana na kilimo, misitu na matumizi mengine ya ardhi.
 
Kuna njia nyingi za kupunguza uchafuzi wa hewa kutoka kwa kilimo. Watu wanaweza kuhamia kwenye lishe inayotegemea mimea na/au kupunguza taka ya chakula, wakati wakulima wanaweza kupunguza methani kutoka kwa mifugo kwa kuimarisha lishe na kuboresha usimamizi wa sehemu za malisho na nyanda. 

TAKA

Uchomaji wazi wa takataka na taka zinazoweza kuoza kuoza katika maeneo yaliyo wazi pia huachilia dioksini hatari, furani, methani na kaboni nyeusi kwenye anga. Ulimwenguni kote, inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya taka huteketezwa wazi. Tatizo hilo ni kubwa sana katika maeneo ya miji na nchi zinazoendelea. Uchomaji wazi wa taka za kilimo na/au za manispaa hufanywa katika nchi 166 kati ya 193.
 
Kuboresha ukusanyaji, kutenganisha na utupaji wa taka hupunguza kiwango cha taka ambazo zimechomwa au kujazwa ardhini. Kutenganisha taka inayoweza kuoza na kuibadilisha kuwa mbolea au nishati kutoka kwa mimea inaboresha rutuba ya mchanga na hutoa chanzo mbadala cha nishati. Kupunguza makadirio ya theluthi moja ya chakula chote ambacho kinapotea au kuharibika pia kunaweza kuboresha hali ya hewa.

VYANZO VINGINE

Sio uchafuzi wote wa hewa unatokana na shughuli za kibinadamu. Mlipuko wa volkano, dhoruba za vumbi na michakato mingine ya asili pia ni changamoto. Dhoruba za mchanga na vumbi  zinatia wasiwasi sana. Chembe ndogo za vumbi zinaweza kusafiri maelfu ya maili kwenye dhoruba hizi, ambazo zinaweza pia kubeba vimelea vya magonjwa na vitu vyenye madhara, na kusababisha matatizo makali na ya kudumu ya kupumua.

Ingawa kusoma kuhusu vyanzo hivi vingi vya uchafuzi wa hewa kunaweza kuonekana kuwa kunataziza mno, kuna hatua tunazoweza kuchukua. 

Ingawa kusoma kuhusu vyanzo hivi vingi vya uchafuzi wa hewa kunaweza kuonekana kuwa kunataziza mno, tunaweza kufanya jambo kuhusu hali hiyo. 

  • Kama mtu binafsi unaweza kupiga kura kwa sauti yako na pesa zako. Unaweza kubadilisha unavyoishi kupunguza matumizi ya mafuta na nishati, kutupa chakula kidogo na kadhalika.
  • Serikali zinaweza kupitisha na kutekeleza viwango vya mazingira vya kiwango cha kimataifa kwa fueli isiyochafua mazingira, na magari yasiyochafua mazingira na yanayotumia nishati vizuri.
  • Miji inaweza kuunda mifumo madhubuti ya usafiri wa umma na mipango ya usafirishaji ambayo inatoa kipaumbele kwa kutembea, matumizi ya baiskeli, na usafiri wa umma. 
  • Wafanyabiashara wanaweza kuchukua hatua moja kwa moja kwa kupunguza uchafuzi wao na kuanzisha teknolojia mpya kutusaidia kuishi bila kuchafua mazingira, bila taka nyingi.

Ikiwa sote tutachukua hatua, tunaweza kupumua kwa urahisi zaidi. Hatuwezi bila wewe.